
Halmashauri ya Mji wa Geita inaudai Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) shilingi bilioni 24.6 za Ushuru wa Huduma ambazo mgodi huo ulitakiwa kuzilipa katika miaka tisa kutoka mwaka 2004 hadi 2014.
Hata hivyo, GGM imepinga madai hayo ikisema kuwa Sheria ya Kodi ya Huduma ilitungwa mwaka 2004 na kuanza kutumika mwaka 2005.
Muwakilishi wa uongozi wa mgodi huo amesema kuwa walitakiwa kulipa dola za Marekani 200,000 na baadaye mwaka 2014 Sheria ilibadilishwa na kutakiwa kuanza kulipia asilimia 0.3 ya mapato yao ya mwaka hivyo kudai kuwa siyo sahihi kudaiwa kiasi hicho cha fedha. Tayari Halmashauri hiyo ya Mji wa Geita imekwishawasilisha hati ya madai kwa uongozi wa mgodi huo na kutoa siku 30 kulipwa dola za Marekani milioni 11.04 (shilingi bilioni 24.6) zikiwa ni malipo ya tozo ya Ushuru wa Huduma.
Suala hilo hilo liliibuliwa na Madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Geita baada ya muwakilishi wa GGM, Joseph Mangilima kuomba ufafanuzi kwa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uongozi juu ya deni hilo.
Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Queen Luvanda alisema deni hilo lilitokana na taarifa iliyotolewa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) baada ya kufanya ukaguzi katika mgodi huo mwaka 2016.
Alisema kuwa ukaguzi huo ulianisha deni hilo ambalo inadaiwa mgodi huo uligoma kulilipa kwa kigezo kuwa Halmashauri haikuwa na Sheria Ndogo ya kudai kodi hiyo.