
Makamu wa rais wa zamani wa Marekani amesema kuwa, kipindi cha urais wa Donald Trump huenda kikamalizika mapema kwa sababu ya kashfa za kimaadili.
Al Gore ambaye alikuwa makamu wa rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton amesema ni miezi sita sasa tangu Donald Trump aposhika hatamu za kuiongoza Marekani lakini inaonekana kuwa kipindi cha uongozi wake kitamalizika kabla ya wakati wake.
Al Gore amekosoa uamuzi wa Trump wa kuiondoa Marekani katika mkataba wa hali ya hewa wa Paris na kuongeza kuwa, ana yakini kwamba licha ya Washington kujiondoa katika mkataba huo lakini miji, majimbo na wakurugenzi wa makampuni ya kibiashara ya Marekani wataendelea kuheshimu majukumu yao kuhusu mkataba huo na kupambana na uharibifu wa mazingira.

Makamu wa rais wa zamani wa Marekani amesema makubaliano ya hali ya hewa ya Paris ni mkataba wa dunia ambayo Marekani pia ni mwanachama wake. Ameongeza kuwa, mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira ni vita vya kimaadili sawa kabisa na vile vya harakati za kiraia.
Wiki iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliutaarifu rasmi Umoja wa Mataifa kwamba, Washington imejiondoa katika makubaliano ya hali ya hewa ya Paris.